CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI,
TAREHE 5 JUNI, 2016 MKOANI DAR ES SALAAM

Ndugu Wananchi;
Leo Watanzania tunaungana na jamii ya kimataifa Duniani kote kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira. Siku hii muhimu huadhimishwa kwa lengo la kukumbushana na kuelimishana umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira, na wajibu wa jamii wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka huu tumeelekeza yafanyike katika kila Mkoa. Hivyo Watanzania kote nchini, Mikoa, Wilaya na vijijini wanaungana kwa pamoja kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuelimishana na kuhamasishana juu ya umuhimu wa kutunza na kuyahifadhi mazingira yetu.
Ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni: “Tulinde Maisha ya Wanyamapori kwa Maendeleo Endelevu” (“Go Wild for Life”). Kitaifa ujumbe huu unahimiza jamii kutambua umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori hususan Tembo na Faru kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Ujumbe huu unatokana na ukweli kwamba wanyama hawa wanakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na uwindaji haramu unaofanywa kwa sababu ya biashara haramu ya pembe zao. Kwa takwimu za 2014, Tanzania inapoteza Tembo elfu kumi (10,000) kwa mwaka na sababu kubwa ni uwindaji haramu. Tunapaswa kwa pamoja kuzuia hali hii ili tuweze kuhifadhi rasilimali zetu tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ndugu Wananchi;
Kaulimbiu ya kitaifa ya Siku ya Mazingira tumeielekeza kwenye kuhifadhi Vyanzo vya Maji ambayo inasema “Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa Letu”. Ujumbe huu unatukumbusha changamoto za mazingira tulizonazo kuhusu uharibifu wa vyanzo vya maji na umuhimu wa maji kwa maisha yetu na viumbe wengine. Uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini ni kero kubwa. Aidha, uharibifu wa Vyanzo vya Maji na mfumo wa maji ni miongoni mwa changamoto za Mazingira zinazoendelea kulikumba Taifa letu. Pamoja na juhudi za Serikali za kukabiliana na changamoto hizo, hatua zaidi zinahitajika kuhakikisha kuwa ufumbuzi wa kudumu unakuwepo.
Tunapoadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, tunapaswa tuchukue hatua za kuhakikisha usafi wa maeneo yetu na kila mmoja wetu ashiriki katika juhudi za usafi wa mazingira. Juhudi thabiti na ushiriki wa kila mmoja wetu katika suala la usafi ndio nguzo kuu ya mafanikio katika kuboresha maisha na afya. Maadhimisho haya pia tuyatumie kukuza uelewa kwa jamii, kuchochea na kuongeza utashi wa kisiasa katika masuala ya kuhifadhi na kusimamia mazingira yetu.
Utafiti katika masuala ya Afya unaonesha kwamba asilimia sitini hadi themanini (60% - 80%) ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali hapa nchini wanaugua magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama. Aidha, kutokana na uchafuzi wa vyanzo vya maji baadhi ya vyanzo hivyo siyo tu vimepoteza uwezo wake wa kutoa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na wanyama bali hata uwezo wa kuwezesha maisha ya viumbe kuishi kwenye vyanzo hivyo umetoweka.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na juhudi zilizochukuliwa kukabiliana na uharibifu wa mazingira ni muhimu ifahamike kwamba mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu, na ndio uhai wa viumbe vyote duniani. Maisha ya binadamu yanategemea ardhi, maji, mimea na hewa. Pamoja na umuhimu huo, tunaendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na kilimo kisichoendelevu kinachofanyika kwenye vyanzo vya maji; vilele na miteremko ya milima; matumizi mabaya ya dawa za kilimo, mifugo na viwanda; kilimo cha umwagiliaji maji kisichoendelevu; uchomaji moto misitu; uchimbaji wa madini usioendelevu; mlundikano wa taka katika maeneo ya mijini na makazi ya watu, n.k. Vile vile, wingi wa mifugo inayozidi uwezo wa malisho husababisha upungufu wa maji na malisho na hivyo kuchangia kuongezeka kwa migogoro baina ya wafugaji na wakulima.
Ongezeko la idadi ya watu hapa nchini kutoka milioni 34.4 mwaka 2002 hadi 44.9 mwaka 2012 ni changamoto ingine inayochochea uharibifu wa mazingira kwa ujumla. Watu wanapoongezeka, mahitaji ya maliasili zetu pia yanaongezeka na taka zinazozalishwa pia zinaongezeka. Mahitaji ya maji, chakula, mazao ya misitu, ardhi ya kilimo n.k. vyote vinaongezeka kwa kuwa wahitaji wanakuwa wengi zaidi.
Ndugu Wananchi;
Kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira unahitaji ushirikiano wa wadau wote kwa ngazi zote. Nitoe wito kwa wananchi wote, vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia, Watendaji wote katika ngazi zote kushirikiana katika kufanya yafuatayo: i) Kutekeleza kikamilifu Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Mtakapofanya hivyo mtapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. ii) Katika kila ngazi pawepo na Mipango bora ya ardhi, Mikakati bora ya kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Mikakati ya kudhibiti uvunaji holela wa misitu na ufugaji usio endelevu. iii) Wizara na Taasisi husika kwa kushirikiana na jamii yote, ziendeleze mafanikio yaliyokwishapatikana kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Mikakati, Mipango, Sheria na Kanuni tulizojiwekea. iv) Tuweke mazingira yetu yawe safi. Usafi wa Mazingira uhusishe kila mtu kuhakikisha taka zinakusanywa na zinatupwa maeneo yaliyotengwa. v) Tupande miti mingi wakati wa msimu wa mvua ili tujihami na kunea kwa hali ya jangwa na mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, kwa mara nyingine, napenda kuushukuru na kuupongeza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa maandalizi mazuri ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira. Nazipongeza tena Halmashauri, Taasisi, Makampuni, Vikundi na Watu binafsi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha maadhimisho haya. Mwisho nivipongeze Vyombo vya habari kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki maadhimisho haya.
Baada ya kusema haya, natamka kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hapa Mkoa wa Dar esSalaam yamefikia Kilele. “Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa Letu”.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Amaizing ✌️✌️❤️
ReplyDelete